Wananchi kote nchini wameshauriwa kutotumia dawa za tiba asili bila ya kupata ushauri kutoka kwa wataalamu ili kutumia kwa kiwango kilichotafitiwa (dozi) cha mimea tiba wanayoitumia kwa ajili ya kutibu afya zao kwakuwa kiwango kingi ama kidogo, vyote vinaweza kuleta madhara katika mwili wa binadamu.
Hayo yamezungumzwa na mtafiti mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Frank Rwegoshora alipokuwa akiwasilisha sehemu ya matokeo ya Utafiti wake wa miaka minne aliyokuwa akifanya juu ya kemikali zilizopo kwenye mimea dawa kulingana na mazingira ya kijiografia na umri wa mmea dawa husika.
Mtafiti huyo amesema waganga wengi wa tiba asili hapo awali walikuwa hawafahamu kuwa mimea dawa ina kemikali na kwamba kemikali hizo ndizo zinazotibu magonjwa na kwa namna hiyo lazima watambue kiasi cha dawa ambacho mgonjwa anapaswa kupewa ili dawa zisilete madhara au kushindwa kutibu kutokana na kumpa mgonjwa dozi ndogo au kubwa.
Rwegoshora amesema kuwa utafiti wake ulijikita kwenye mmea dawa wa Mvunjakongwa “Synadenium glaucescens Pax” unaopatikana maeneo mengi ya Tanzania.
“Mimea inazo kemikali nyingi na una sehemu mbalimbali kama vile mizizi, majani na magome ambazo zinatumika kutibu, nami utafiti wangu unahusika na kemikali za mmea huu lengo kubwa ni kuainisha kemikali zilizomo kwa mtiririko wa namna gani na umri wa mmea huu wa Mvunjakongwa ili tusijejikuta tuna vuna ile miti iliyokomaa peke yake kumbe tungeweza kupata matokeo mazuri hata kwenye ile miti midogo”, alisema Rwegoshora.
Watafiti wakifanya vipimo vya sampuli walizokusanya
Akielezea utafiti huo ambao umehusisha Mvunjakongwa kutoka mikoa ya Njombe, Morogoro na Tanga amesema kuwa utafiti wake umevumbua kemikali mpya kabisa duniani pamoja na nyinginezo nyingi hadi ngazi ya maumbo kamili (‘chemical structures’).
Kwa marejeo ya tafiti nyingine duniani amesema kuwa mmeo huo kemikali zake zinaweza kuondoa sumu mwilini pamoja na kufanya vizuri kwenye magonjwa ya kansa mbali mbali pamoja na kisukari.
Aidha amewataka wananchi kuwa na subira juu ya matokeao hayo ya tafiti wasianze kuvuna na kuuza dawa moja kwa moja wasubiri matokeo ya kina juu ya mmea huo.
“Tumeweza kugundua kemikali nyingine mpya kabisa ambayo haijawahi gundulika kokote duniani ambapo awali ziligundulika kemikali nne tu lakini kwa sasa kipo kilichoongezeka ambacho ni sifa pia kwa nchi yetu”, alisema Rwegoshora.
Aidha Rwegoshora ameongeza kuwa taarifa nyingine zilizopo juu ya mimea hiyo huwa wanatumia kwaajili ya kutibu mafindo findo ya ng’ombe, virusi vya ukimwi (VVU), kifua kikuu na kikohozi kikali, kuzungushia kwenye ghala za nafaka kwa ajili ya kuzuia vijidudu, kutibu tumbo ambapo kuchanganywa na vitu kama asali, pamoja na kutibu matumbo ya hedhi kwa wanawake.
Mmea wa mvunjakongwa
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Prof Hamisi Malebo amepongeza kazi kubwa ya utafiti inayofanywa na watafiti kutoka SUA na kwamba tafiti zao zinasaidia katika kuboresha namna wataalamu wa tiba asili wanavyoweza kutoa tiba kisayansi.
“Mradi huu wa GRILI umefanya kazi kubwa sana katika kuboresha kazi za waganga wa tiba asili nchini katika maeneo mbalimbali ya ufungashaji, usindikaji wa bidhaa zao na maswala muhimu ya masoko ili waweze kufikia viwango vinavyokubalika kimataifa” Alisema Prof. Malebo
Prof. Malebo amewataka watafiti na taasisi za utafiti nchini kufanya utafiti wa kina ili kuleta matokeo ya kisayansi kwani kwa sasa kumekuwa na mwamko mkubwa wa jamii katika matumizi ya dawa za asili hivyo ni lazima sayansi itumike katika kupata majibu sahihi ya matumizi ya mimea dawa nchini na kama zinavyofanya nchi zingine kama vile India na China na kunufaisha jamii na taifa.
Prof. Malebo amesema Baraza hilo tayari limesajili dawa za asili ambazo zinaonyesha uwezo mkubwa wa kupamabana na Virusi vya Ukimwi na ambazo pia zinaonyesha uwezo wa kuinua afya na kinga za watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.
Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Prof Hamisi Malebo akizungumza juu ya utafiti huo
Mradi wa utafiti wa kuongeza ubunifu katika mimea dawa ili kuboresha Maisha (GRILI) ulianza mwaka 2010 unawashirikisha wadau mbalimbali kama vile Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Copenhagen cha nchini Denmark, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Taasisi ya Dawa Asili Muhimbili (ITM), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali(GCLA), Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Binadamu (NIMRI), Chuo Kikuu cha Sayansi Nelson Mandela (NM-AIST), Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Waganga wa tiba asili na watumiaji wa mimea dawa nchini Tanzania kwa ufadhili wa shirika la maendeleo la Denmark DANIDA.