Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kimeahidi kufanya kazi bega kwa bega na wadau mbalimbali waliopo katika Mnyororo wa Thamani wa Bidhaa za Tiba Asili kwaajili ya kuibua Bunifu na kupata suluhisho la Kisayansi kuhusu changamoto zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa biashara ya bidhaa za Mimea Dawa nchini.
Hayo yamebainishwa siku ya Jumatatu Agosti 29, 2022 na Mkurugenzi wa Uzamili, Utafiti na Uhaulishaji wa Teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Profesa Esron Karimuribo wakati akimuwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma na Tafiti Profesa Maulid Mwatawala ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Kwanza la Kisayansi la Tiba Asili Tanzania la siku mbili lililofanyika SUA Kampasi Kuu ya Edward Moringe Sokoine.
Amesema uwepo wa Kongamano hilo la Kisayansi kuhusu Tiba Asili ya Mwafrika lililowakutanisha Wadau mbalimbali waliopo katika Mnyororo wa Thamani wa Bithaa za Tiba Asili wakiwemo Wakulima wazalishaji, Wavunaji, Watengenezaji, Wauzaji wa jumla na rejareja , Taasisi zinazosimamia Ubora, Watunga Sera na Watafiti upo kwenye moja ya majukumu na malengo ya uanzishwaji wa SUA.
Profesa Karimuribo amesema wanaamini lengo la Kongamano hilo ni kuibua Bunifu na kupata suluhisho la Kisayansi kuhusu changamoto zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa biashara ya Bidhaa za Mimea Dawa nchini ili iwe endelevu na iweze kutoa mchango mkubwa kwenye kipato cha Wananchi kwa ujumla.
” Tunathamini sana mchango wa Sekta hii na tunaamini tukishirikiana kwa pamoja tutafika mbali hivyo nasisitiza katika swala la Ubunifu ili kuweza kuwa na Dawa Asili zilizopo katika mfumo ambao unaweza kuupeleka kwenye “Pharmacy” na ambapo tutaweza kujua kilichopo ndani, dozi ni kiasi gani n.k watafiti hawa wazidi kujiongeza na kufanya Dawa hizi za Asili kuwa katika muundo wa kama dawa nyingine tunazotumia ” amesema Profesa Karimuribo
Aidha Profesa Karimuribo amewahakikishia wadau wa Kongamano hilo la Kwanza la Kisayansi la Tiba Asili Tanzania kuwa SUA kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania itakuwa bega kwa bega nao katika kuhakikisha kuwa yatokanayo na Kongamanola hilo yanapewa kipaumbele katika kazi zao za Utafiti, Mafunzo na kuwa endelevu ili kuboresha Bidhaa hizo za Tiba Asili.
Kwa upande wake Dkt P. P Mohamed kutoka Wizara ya Afya amekiomba Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kuwasaidia kufanya Utafiti wa namna ya kulima na kupanda Miti Dawa katika kiwango kinachokubalika vilevile kutokana na Idara Maalum walizonazo chuoni hapo kama vile Kilimo, Udongo Pamoja na Misitu awana budi kuwasubiri mpaka pale watakapoamua kuanzisha Kiwanda ambacho kitawasaidia UBIWATA katika Upatikanaji rahisi na bora wa Mimea dawa.