Watumishi wa SUA kampasi ya Solomon Mahlangu wahimizwa kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao

Watumishi wa SUA wamehimizwa kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu na utendaji kazi ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wanafunzi na wanajumuiya wa Chuo

Wito huo umetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda wakati akiongea na watumishi wa Chuo, Kampasi ya Solomon Mahlangu akiwa katika ziara ya kutembelea Kampasi na Ndaki mbalimbali kwa ajili ya kusikiliza changamoto na kuelezea mipango ya Chuo kwa mwaka ujao wa masomo 2023/2024.

 Prof. Chibunda akiwa ameambatana na Menejimenti ya Chuo hicho, amehimiza kila mtumishi kuona umuhimu wa kushirikiana kiutendaji bila ya kushushiana heshima wakati inajengwa nyumba moja.

 “Tuendelee kufanya kazi kwa umoja, hakuna haja ya kushindana kwani kila mmoja ana mchango katika utoaji wa huduma kwenye eneo lake,” alisema Prof. Chibunda.

 Aidha, Makamu huyo wa Chuo amesisitiza kuwa Chuo kitaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa Chuo hicho pamoja na kuboresha mazingira ya utoaji wa taaluma ili kuendelea kuifanya SUA kuwa bora katika kuandaa wahitimu wenye uwezo mkubwa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

Kwa upande wake, Kaimu Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi Dkt. Beda Mwang’onde amemshukuru Makamu Mkuu wa Chuo kwa kutenga muda kuzungumza na watumishi akisema kikao hicho kitakuwa chachu katika kuongeza ari ya utendaji kazi kwa watumishi.

Dkt. Neema Sumari ni Mhadhiri na miongoni mwa wafanyakazi walioshiriki katika kikao hicho akiongea na SUAMEDIA amebainisha kuwa kikao hicho kimekuwa na tija kwani changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi zimepatiwa ufumbuzi na nyingine zimechukuliwa kwa ajili ya kutafuta suluhu zaidi.

 Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo inaendelea na ziara ya kutembelea Kampasi na Ndaki mbalimbali kwa minajili ya kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyakazi wa Chuo hicho pamoja na kupanga mikakati ya pamoja ya namna ya kuboresha utoaji wa elimu kwa mwaka ujao wa masomo.

 

 

Credit: SUA Media

Related Posts